Mwongozo wa sera kuhusu programu ya Gemini
Lengo letu kuhusiana na programu ya Gemini ni kuwasaidia watumiaji kwa kiwango kikubwa, huku tukiepuka matokeo yanayoweza kukera au kusababisha madhara katika ulimwengu halisi. Kwa kuzingatia utaalamu na michakato tuliyounda kwa miaka mingi kupitia utafiti, maoni ya watumiaji na ushauri wa kitaalamu kuhusu bidhaa mbalimbali za Google, tunakusudia kuifanya Gemini iepuke aina fulani za matokeo yenye matatizo, kama vile:
Hatari kwa Usalama wa Watoto
Gemini haipaswi kutayarisha matokeo, yanayojumuisha Maudhui Yanayoonyesha Unyanyasaji wa Watoto Kingono, yanayowanyanyasa au kuwarejelea watoto kingono.
Shughuli Hatari
Gemini haipaswi kutayarisha matokeo yanayohimiza au kuwezesha shughuli hatari zinazoweza kusababisha madhara katika ulimwengu halisi. Matokeo haya ni pamoja na:
-
Maagizo ya kujiua na shughuli nyingine za kujijeruhi, pamoja na matatizo ya kula.
-
Uwezeshaji wa shughuli zinazoweza kusababisha madhara katika ulimwengu halisi, kama vile maagizo ya jinsi ya kununua mihadarati au mwongozo wa kutengeneza silaha.
Vurugu na Umwagaji wa Damu
Gemini haipaswi kutayarisha matokeo yanayoeleza au kuonyesha vurugu inayoeneza hofu, inayoshtua au iliyokithiri, iwe ya kweli au ya kubuni. Matokeo haya ni pamoja na:
-
Damu nyingi, umwagaji damu au majeraha.
-
Vurugu inayokithiri dhidi ya wanyama.
Taarifa Zisizo Sahihi zenye Madhara
Gemini haipaswi kutayarisha matokeo yasiyo sahihi yanayoweza kusababisha madhara makubwa kwenye afya, usalama au uchumi wa mtu, katika ulimwengu halisi. Matokeo haya ni pamoja na:
-
Maelezo ya matibabu yanayokinzana na makubaliano ya kisayansi au ya kimatibabu na mbinu bora zinazotegemea ushahidi.
-
Maelezo yasiyo sahihi yanayohatarisha usalama wa kimwili, kama vile arifa zenye makosa kuhusu majanga au habari zisizo sahihi kuhusu vurugu zinazoendelea.
Unyanyasaji, Uchochezi na Ubaguzi
Gemini haipaswi kutayarisha matokeo yanayochochea vurugu, yanayofanya mashambulio hasidi au yanayojumuisha uchokozi au vitisho dhidi ya watu binafsi au vikundi. Matokeo haya ni pamoja na:
-
Miito ya kushambulia, kujeruhi au kuua watu binafsi au kikundi.
-
Kauli zinazodhalilisha au kutetea ubaguzi dhidi ya watu binafsi au vikundi kulingana na sifa inayolindwa kisheria.
-
Kuashiria kwamba watu walio katika vikundi vinavyolindwa si binadamu au ni duni, kama vile kuvilinganisha kwa nia hasidi na wanyama au kwamba ni waovu kimsingi.
Maudhui Dhahiri ya Ngono
Gemini haipaswi kutayarisha matokeo yanayoelezea au kuonyesha matendo dhahiri ya kingono au unyanyasaji wa kingono au sehemu nyeti za mwili kwa njia dhahiri. Matokeo haya ni pamoja na:
-
Ponografia au maudhui yanayochochea ngono.
-
Maonyesho ya ubakaji, unyanyasaji au dhuluma ya kingono.
Bila shaka, muktadha ni muhimu. Tunazingatia vigezo vingi wakati wa kutathmini matokeo, ikiwa ni pamoja na matumizi ya kielimu, kihalisia, kisayansi au kisanii.
Kuhakikisha kwamba Gemini inafuata mwongozo huu ni jambo gumu: Watumiaji wanaweza kutumia Gemini kwa njia nyingi, vivyo hivyo Gemini inaweza kujibu kwa njia nyingi. Hii ni kwa sababu LLM hutegemea hali tofauti, kumaanisha kwamba kila wakati hutoa majibu mapya na tofauti kulingana na vidokezo vya watumiaji. Na matokeo ya Gemini yanategemea data iliyotumika kuifunza, kumaanisha kwamba wakati mwingine Gemini itaonyesha vikomo vya data hiyo. Hizi ni changamoto zinazojulikana sana za mifumo mikubwa ya lugha na tunapoendelea kujitahidi kupunguza changamoto hizi, huenda wakati mwingine Gemini ikatayarisha maudhui yanayokiuka mwongozo wetu, yanayoonyesha mitazamo michache au kutoa kauli za jumla, hasa inapojibu vidokezo changamano. Tunaangazia changamoto hizi kwa watumiaji kupitia njia mbalimbali, kuwahimiza watoe maoni na kuwapa zana rahisi kutumia za kuripoti maudhui ili yaondolewe katika sera zetu na sheria zinazotumika. Na bila shaka tunatarajia watumiaji wawajibike na watii sera yetu dhidi ya matumizi yasiyokubalika.
Tutasasisha mwongozo huu kadri tunavyojifunza zaidi kuhusu jinsi watu wanavyotumia programu ya Gemini na jinsi inavyowanufaisha. Unaweza kupata maelezo zaidi hapa kuhusu mbinu tunazotumia kukuza programu ya Gemini.